Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa), kimetangaza kuwa Mwanamichezo Bora wa Tanzania kwa mwaka 2010 atazawadiwa gari.
Akizungumza Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto amesema wanamichezo wengine watakaoshinda kwenye kila mchezo watazawadiwa Sh milioni moja kila mmoja.
Pinto alisema kuwa wameamua kumpa gari mshindi kama njia mojawapo ya kumpongeza kutokana na mafanikio yake, lalini pia kuwapa changamoto wengine ya kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ili siku za usoni nao wapate zawadi hizo.
“Tumeamua kutoa gari mpya aina ya Toyota GX 100, yenye thamani ya Sh milioni 13, tunaamini zawadi hii inaweza kusaidia wanamichezo kuona jinsi gani tunavyowathamini,” alisema Pinto.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa karibu vyama 15 vya michezo mbalimbali, vitapewa tuzo kwa wanamichezo wao waliofanya vizuri mwaka 2010 na kwamba kati ya vyama hivyo kuna vingine michezo yao inachezwa na jinsia mbili, hivyo idadi ya tuzo zitazidi 30.
“Michezo kama wavu, soka, mpira wa mikono, gofu, tenisi na mingine inachezwa na wanaume na wanawake, hivyo lazima uwe na tuzo kwa pande zote mbili.
“Pia kutakuwa na tuzo nyingine nne, ambazo ni Tuzo ya Heshima kwa aliyetoa mchango kwenye michezo, Tuzo ya Mwanamichezo Bora Chipukizi, Tuzo ya Mtanzania anayecheza nje ya nchi na Tuzo ya Mwanamichezo wa Nje anayecheza Tanzania,” alisema.
Alisema baada ya kuwapata wanamichezo bora wa kila mchezo, ndipo miongoni mwao atatoka Mwanamichezo Bora wa Tanzania kwa mwaka 2010, ambao wote watazawadiwa Mei 6, mwaka huu kwenye sherehe zitakazofanyika Hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam.
Naye Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) inayodhamini tuzo hizo, Teddy Mapunda alisema, licha ya kupewa zawadi ya gari, pia mshindi atalala kwenye Hoteli ya Movenpick kwa siku moja katika chumba cha hadhi ya daraja la juu.
Alisema kampuni yake itaendelea kushirikiana na Taswa kuhakikisha kuwa tuzo hiyo inakuwa bora na ya aina yake hapa nchini.
Wanamichezo wengine waliotwaa tuzo hiyo kuanzia mwaka 2006 ni Samson Ramadhan, Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao ni wanariadha na Mwanaid Hassan (2009).
Zawadi ya juu ya Mwanamichezo Bora ilitolewa mwaka jana, ambapo mshindi alipata Sh 700,000 kwa ushindi wa jumla na ile ya mwezi alipata Sh 300,000 hivyo kumfanya aondoke na Sh milioni moja.
No comments:
Post a Comment