Friday, April 8, 2011

taswa fc yaalikwa Arusha

Timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo nchini, Taswa Fc imealikwa mkoani Arusha kwenda kutetea ubingwa wao wa Taswa -Arusha sports bonanza.

Taswa FC ambayo ni mabingwa mara mbili, imepokea taarifa kutoka kwa muandaaji wa bonanza hilo, Mussa Juma na imepania vilivyo kulichukua kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo.

Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto Omary alisema kuwa bonanza hilo limepangwa kufanyika Mei 8 na kikosi cha wachezaji 24 na viongozi sita wa timu hiyo kinatarajia kuondoka jijini Mei 5 kuelekea mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Majuto alisema kuwa wakiwa njiani, watacheza mechi moja mkoani Kilimanjaro (Moshi mjini) dhidi ya maveterani wa mkoa huo na baadaye kuondoka usiku kuelekea Arusha na kuweka kambi ya siku mbili (Mei 6 na Mei 7) kabla ya kuanza kazi ya kutetea ubingwa wao.

"Tupo katika maandalizi mbali mbali pamoja na kusaka wadhamini, kama unavyojua tunategemea sana wadhamini ili kufanikisha safari yetu, hivyo tunaomba wadhamini watupige tafu," alisema Majuto.

Alisema kuwa wakiwa njiani, Taswa Fc itasimama Segera na kucheza mechi moja siku ya Mei 9 na kuondoka usiku huo huo kurejea DSM.

Kiongozi huyo aliwataka wachezaji wote kufanya maandalizi ya kina ili kuweza kutimiza wajibu wao katika mashindano hayo.

No comments: