Tuesday, April 19, 2011

Mwasika ' out' Yanga, Taifa Stars kwa miezi 6

MCHEZAJI tegemeo wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars, Stephano Mwasika uenda asicheze mechi zilizobakia za kufuzu kombe la Mataifa ya Afrika kutokana na kuwa majeruhi.

Mwasika ambaye alicheza mechi dhidi ya Afrika ya Kati akitokea benchi na kuiwezesha timu hiyo kushinda mabao 2-1 anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa goti au misuli ya meniscus na anatarajiwa kuwa nje kati ya miezi minne na sita.

Upasuaji huo umepangwa kufanyika nchini India na lini utafanyika itategemea mipango ya klabu yake ya Yanga ambayo ndiyo yenye jukumu la mwisho la matibabu ya mchezaji huyo kwa mujibu wa taratibu za Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA).

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Jan Poulsen alisema kuwa ni pigo kwa timu yake kwani hakumjumuisha mchezaji huyo kwenye timu inayokwenda kucheza mechi ya kimataifa dhidi ya Msumbiji ili kupisha matibabu yake.

“Nimepata taarifa kuwa atakwenda India, hii ina maana kuwa atakuwa nje muda mrefu, kuwepo kwake katika timu hii itategemea zaidi nafuu yake, sina jinsi zaidi ya kutafuta mchezaji ambaye ataweza kuziba pengo lake,” alisema Poulsen.

Poulsen alisema kuwa alimjumuisha Mwasika katika kikosi ambacho kilitarajia kupambana na Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Juni, lakini kwa sasa hali imekuwa tofauti.

Daktari wa timu ya Taifa, Juma Mwanandi Mwamkemwa alisema kuwa lazima mchezaji huyo afanyiwe upasuaji na madaktari bingwa wapo nchini India na anaamini ataendelea kucheza baada ya kupona.

“Kwa kifupi, baada ya kupasuliwa atatakiwa kukaa si chini ya miezi minne ili aanze mazoezi ya taratibu huku akiangaliwa kwa undani zaidi na nadhani itachukua kati ya mwezi mmoja na nusu ili kurejea hali yake ya kawaida baada ya miezi minne,” alisema Mwamkemwa.

Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu kuwa ni masikitiko makubwa timu yao kumkosa Mwasika licha ya kuwa wachezaji wao wako katika kusherehekea sikukuu.

No comments: