Monday, March 14, 2011

MECHI YA SIMBA VS TP MAZEMBE: NI VITA YA MWALIMU DHIDI YA MWANAFUNZI

KOCHA Mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Phiri ameifananisha mechi yao dhidi ya Mabingwa watetezi, TP Mazembe sawa na vita kati ya Mwanafunzi na Mwalimu.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Arusha, Phiri alisema kuwa wanajua kuwa wanapambana na timu kubwa yenye historia mpya kabisa katika soka la Afrika na lengo lao litabakia palepale la kutafuta ushindi.

Alisema kuwa TP Mazembe ni mabingwa watetezi kwa mara ya pili mfululizo na klabu pekee katika bara la Afrika iliyoweza kufika fainali ya klabu bingwa ya Dunia kwa kuzitoa timu kongwe duniani.

“Simaanishi kuwa hatuwezi kuwatoa TP Mazembe, hapana, kwani hata Mwalimu anaweza kushindwa kwa mwanafunzi, tunakwenda kushindana na vile vile kusaka ushindi,” alisema Phiri.

Alisema kuwa historia mara nyingi uwa inatengenezwa kwa mechi mfano dhidi ya TP Mazembe kwani wadau wengi wa soka wanadhani kuwa tutafanya vibaya kutokana na historia ya timu hiyo kwa soka la Afrika hivi sasa.

“Tunajiandaa kwenda kushindana, kupigana mpaka tone la mwisho, naamini tutafikia lengo letu, ubora wa TP Mazembe si wa kubeza na naamini wachezaji wangu watafanya kile kinachotarajiwa na wadau wengi kama ilivyokuwa kwa timu ya Zamalek ya Misri mwanzoni mwa miaka ya 2000,” alisema Phiri.

Alisema kuwa anawajenga wachezaji wake kwa kisaikolojia, kiufundi na kujuzi kwa ajili ya mechi hiyo ambayo inasubiriwa na mashabiki wengi wa soka Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Alifafanua kuwa kambi yake imezidi kuhimarika na hasa baada ya kupona kwa Mussa Hassan Mgosi na maendeleo mazuri ya Emmanuel Okwi ambaye alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa tumbo.

“Pia Patrick Ochan ni mgonjwa, Echessa (Hillary) anaendelea vizuri na Owino (Joseph) naye anaendelea vizuri, uwepo wao katika timu utajulikana Alhamis na hasa kutegemea repoti ya daktari wetu,” alisema.

No comments: