TIMU ya Mwananchi FC imeendelea kutamba katika mechi zake baada ya kuifunga timu ya New Habari Corporation mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Shekilango jijini.
Hii ni mara ya pili kwa Mwananchi FC kuifunga New Habari FC ambapo kwenye mashindano ya Airtel Media Day, Mwananchi FC iliichabanga Habari mabao 4-0.
Mwanachi FC ilifunga bao lake la kwanza kupitia nahodha wake, Majuto “Ronaldo de Lima” ikiwa ni bao la historia katika ulimwengu wa soka.
Majuto alifunga bao hilo mara baada ya mpira kuanza, akipiga shuti tokea katikati ya uwanja na kufunga bao hilo. Bao hilo liliwachanganya sana wachezaji wa New Habari baada ya kunyong’onyeshwa na makosa ya kipa wao.
Wakati New Habari FC wakitafakari kufungwa bao hilo, walijikuta wakipigiliwa ‘msumari’ mwingine kupitia Majuto baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Salum Jaba.
New Habari FC nusura wafunge bao katika dakika 35 kupitia Kulwa Karedia , lakini shuti lake liliokolewa na kipa wa Mwananchi FC, Ibrahim Bakari huku mabeki wake, Sweetbert Lukonge, Jaba, Andrew Kingamkono, Thomas Balele na Sosthenes Nyoni wakifanya kazi nzuri ya kulinga lango lao lisifungwe.
Mwananchi FC ilianza kipindi cha pili kwa kasi na kufunga bao la tatu kupitia kwa Calvin Kiwia baada ya pande safi la Majuto ambaye alishirikiana vizuri na Abdallah Masoud. New Habari FC walifunga bao la kufuta machozi kupitia kwa Karedia aliyepata pasi safi ya Mohamed Mharizo.
No comments:
Post a Comment