Tuesday, March 15, 2011

'SABABU ZA TASWA FC KUTOCHEZA KOVA CUP HIZI HAPA

Uongozi wa timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo nchini, Taswa FC umesema kuwa haujatokea katika mechi za mashindano ya Kova Cup kutokana na kutopata ratiba.

Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto Omary alisema kuwa taarifa za kucheza mechi yao ya kwanza walizipata siku ya Jumapili saa 9.00 alasiri baada ya kupigiwa simu na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo, Bw. Chonya na ilikuwa vigumu kwao kuifanyia kazi taarifa ya njia ya simu.

Majuto alisema kuwa katika mazungumzo hayo, njia pekee ya kuwashirikisha wao katika mashindano hayo ni kwa kutuma tarifa au ratiba nzima ya mashindano hayo masaa 48 kabla ya mchezo kwani wachezaji wao wote ni waandishi wa habari na wanahitaji kuombewa ruhusa ili kucheza mechi hizo.

Alisema kuwa taarifa ya Chonya ilikuwa ikiwataka Taswa FC kucheza mechi yake saa 8.00 mchana, hali ambayo ni vigumu kwa waandishi wa habari kuwatoa katika maeneo yao ya kazi ili kwenda kucheza mechi hizo.

“Waandishi au wachezaji wetu wanatakiwa kuripoti maenoe yao ya kazi kuanzia saa 7.00 mchana, hata magari ya kubeba waandishi hufika Idara ya Habari kuanzia saa 7.00 mchana, mfano Waandishi wa Mwananchi Communications Limited (MCL) wao wanatoka katika majukumu yao saa 7 na kurejea makao makuu Tabata Relini, New Habari nao hivyo hivyo, wao wanatatoka Maelezo saa 7.30 mchana kuelekea Sinza, The Guardian Limited nao uondoka saa 7.00, je watafika maeneo yao ya kazi saa ngapi na kucheza mechi saa 8.00?,” alihoji Majuto.

Alifafanua kuwa endapo wangekuwa na ratiba, ingekuwa rahisi kuwaombea ruhusa wachezaji wao ili kufanya kazi mapema na kuwahi mechi hizo.

“Hatuna lengo baya kama baadhi ya wajumbe wa Kamati ya mashindano wanavyodhani, timu yetu ipo kimashindano zaidi na ndiyo maana tumeshinda vikombe vingi sana hapa Dar na Arusha,” alisema.

No comments: